VIONGOZI WA DINI DHIDI YA MASUMBWI MJENGONI

VIONGOZI Madhehebu ya Dini wanaendelea kukerwa na vituko mbalimbali vikiwemo mipasho na hata kutishia kupigana ambavyo vimekuwa vikionyesha na baadhi ya Wabunge katika vipindi vya Bunge mjini Dodoma.
Viongozi hao walionyesha hisia za kero hizo mbele ya waumini wa kanisa la Andrea Mtakatifu Anglikani Parish ya Veyula walipokuwa wamehudhuria uzinduzi wa jengo la kuabudia lililopo kati kijiji hicho kata ya makutupola manispaa ya Dodoma.

Askofu wa Anglikan Dayosisi ya kati [DCT] Godfrey Mdimi Muhogolo alisema wabunge wamechaguliwa na wananchi kutokana na kuaminiwa sasa inashangaza kuona kuwa badala ya kufanya uwakilishi waliotumwa wanageuka kuwa wapashanaji, kutukanana na kutishiana.
Muhogolo alisema wananchi wanakuwa na matumaini ya changamoto na yote wanayowatuma wabunge yafikishwe bungeni ili ikiwezekana serekali iyafanyie kazi badala yake inakuwa kinyume bunge linageuzwa kuwa jukwaa la siasa na ulingo wa masumbwi ambao kabla ya wahusika kupigana huanza kwa kutambiana.

Aliongeza kuwa wabunge waliochaguliwa na wananchi ni wasomi kuliko mabunge yaliyotangulia hivyo kama wao wakianzisha fujo bungeni wananchi wao itakuwaje majimboni mwao na cha kusikitisha zaidi wengi wao ni vijana wenye nguvu wanaotegemewa sana na Taifa hili.
“Mimi kama askofu naona hayo yote yanatokana na ukosefu wa hekima, Busara na maadili na ni ngumu kuendesha nchi kwa kutumia nguvu badala ya hoja, usomi wote ni bure hasa kwa vijana heshima ya mtu haipotezwi na Siasa kila mtu afanye wajibu wake ipasavyo ili kurudisha imani ya watanzani kwenye Bunge lake’’, alisema Muhogolo

Nae Mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Chamwino Shekh Said Abubakar Gantana mualikwa katika uzinduzi huo wa kanisa alisema Vitendo hivyo vya kubishana na kutukanana ni vya aibu kwa watanzania na pia kuaibisha viaongozi wao wa Dini kutokana na wabunge wote kushiriki kwenye madhehebu mbalimbali.

Aliwataka wabunge na uongozi mzima wa Bunge kuiga mfano wa viongozi wa Dini ambao wamekuwa wakishirikiana katika mambo mbalimbali katika jamii ili kuendelea kuijenga amani na kuimalisha umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi wa nchi hii waliotangulia akiwemo Hayati Nyerere.
Jengo hilo la kanisa, nyumba ya utumishi,Vyoo Pamoja na samani viligharimu zaidi ya 194 MIL walizolipwa ili kupisha mradi wa Barabara ya Dodoma Arusha unaoendelea kwa kiwango cha lami.

Katibu wa kamati ya ujenzi Marry Nghambala alisema walitumia 173,537,950 kujengea na kununua samani za kanisa, ujenzi wa nyumba ya utumishi ambayo haijakamilika ilitumia 14,466,100 na ujenzi wa vyoo na nyumba za uani kwenye nyumba ya utmishi 6,730,100 na jumla yake ikiwa 194, 734, 150.