WANANCHI WASISITIZWA KUTUNZA MIUNDOMBINU

Wakazi wa kitongoji cha Msangalalee kata ya Dodoma Makulu Manispaa ya Dodoma wametakiwa kuilinda na kuitunza miundombinu ya maji safi iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mwenyekiti wa kitongoji hicho William Chacha wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kitongoji hicho.
Chacha alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu ambao huwa wanaharibu miundombinu ya maji kwa makusudi na kusababisha adha ya maji katika eneo hilo.
Alimtaka kila mtu kuwa mlinzi wa miundombinu ya hiyo ili huduma hiyo muhimu iwe endelevu kwa kupatikana kila wakati kwaa jili ya manufaa ya kila mmoja.
“Nimepata taarifa kuwa kuna watu wanang’oa mabomba ya maji na kwenda kuyauza kama vyuma chakavu, hilo ni kosa kisheria na kama tukikubaini tutakufikisha mahakamani kwa kosa la uharibifu wa miundombinu ya maji ambapo adhabu yake utaijua hukohuko mbele,” alisema Chacha.
Aliongeza, ni jukumu la kila mwananchi kulinda mabomba hayo ya maji safi kwani ndiyo chanzo pekee cha majisafi katika kitongoji hicho ambacho kimeanza kupata huduma ya majisafi mwaka huu tangu uhuru.
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho Lesca Chedego aliipongeza mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini hapa (DUWASA) kwa kuwafikishia huduma hiyo muhimu ya maji wakazi wa kitongoji hicho.
Kitongoji cha Msangalalee kimeanza kupata huduma ya majisafi tangu mwezi wa sita mwaka huu ambapo gharama za mradi huo ziligharamiwa na Duwasa kwa kuweka vituo (Domestic Points (DP)) 6 katika kitongoji hicho.