Mwanza. Shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Aphonce Mawazo aliyeuawa wiki iliyopita iko katika sintofahamu baada ya chama hicho kudai kuzuiwa na polisi kuuchukua mwili huo katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) ulikohifadhiwa.
Viongozi wa kitaifa wa Ukawa na Chadema wakiongozwa na
Mwenyekiti, Freeman Mbowe akiambatana na aliyekuwa mgombea urais, Edward
Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, wakurugenzi wa Chadema
na wabunge wa upinzani waliwasili jijini Mwanza, lakini hadi tunakwenda
mitamboni hawakuwa wamechukua mwili huo.
Taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari,
Tumaini Makene baadaye jioni ilisema vikao vilikuwa vinaendelea na kuwa
taarifa za kina zingetolewa baadaye.
Viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa, walifika BMC jana saa
5.35 asubuhi kuuchukua mwili, lakini hawakufanikiwa na wakaondoka
wakieleza kuwa wanakwenda kufanya mazungumzo kujadili suala hilo.
Makene alisema: “Baada ya viongozi hao kuwasili na kupewa
taarifa za awali kuhusu maandalizi ya ratiba ya utoaji wa heshima za
mwisho kwa Kamanda Mawazo, wamesikitishwa sana na kitendo cha Jeshi la
Polisi mkoani Mwanza kuzuia shughuli hiyo kufanyika jijini humo.”
Akizungumzia kwa nini Mawazo aagwe Mwanza na baadaye Geita,
Makene alisema mbali ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita,
pia alikuwa kiongozi wa Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha mikoa ya
Kagera, Mwanza na Geita.
Msimamo wa polisi
Hata hivyo, polisi walikanusha madai ya kuwazuia Chadema
kuchukua mwili huo lakini wakasisitiza kuwa wamezuia shughuli za kuaga
mwili huo zilizopangwa kufanyika katika ofisi za Kanda ya Ziwa za chama
hicho.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema
wamefanya mazungumzo na baba mdogo wa marehemu, Mchungaji Charles Lukiko
kuwa mwili huo watauchukua kesho (leo) na kwenda kuzika mkoani Geita.
“Sisi hatujawazuia Chadema kuchukua mwili wa Mawazo, ila
wao wameingiza mambo ya kisiasa, tunachosema polisi ni kwamba hatutaki
shughuli za kuaga mwili huo zifanyike mkoani hapa, wala mkusanyiko wa
aina yoyote.”
Mkumbo alisema wamezuia mikusanyiko ya aina yoyote kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Baadaye Mchungaji Lukiko alisema familia itauchukua mwili
wa marehemu kati ya leo na kesho kutoka Bugando na kuupeleka moja kwa
moja Geita kwa ajili ya mazishi.
“Bado kuna mvutano, Chadema wapo kwenye vikao vyao,
wanataka kuuaga mwili wa mwenzao, lakini na sisi kama familia
tunatarajia kati ya Jumapili au Jumatatu tutauchukua. Kwa sasa siwezi
kusema zaidi ya hapo,” alisema Mchungaji Lukiko.
Shughuli hizo za kuaga mwili zilitarajiwa kufanyika jana kwenye Viwanja vya Furahisha au Ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa.
Awali, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema,
Kigaila Benson alisema: “Tunashangaa polisi kutuzia kuuga mwili wa
Mawazo, tulikubaliana kwamba mwili utaagwa katika ofisi za Kanda, lakini
wametugeuka na kutuzuia kufanya hivyo utadhani sisi ni wahalifu.
“Mawazo hajafa kwa kipindupindu, wala hatuendi kula chakula
tunataka tumuage ndugu yetu, wanavyotumia nguvu kubwa sijui inaashiria
kitu gani, ni jambo la kusikitisha kwani angekuwa kafa mtu wa upande wa
pili angeagwa na ulinzi angepewa.”
Mkurugenzi wa Chadema Kanda ya Ziwa, Peter Makere alisema
Chadema ni jeshi kubwa zaidi na kwamba kwa vyovyote lazima mwili wa
mwenzao uagwe kabla ya kwenda kuzikwa Geita.
Ulinzi mkali kila kona
Jana, Jiji la Mwanza lilipambwa na askari polisi waliyokuwa
na sare na waliokuwa wamevalia kiraia kila kona baadhi yao wakiwa
wamebeba silaha za moto na wengine mabomu ya machozi na wengine wakiwa
na mbwa.
Polisi walitanda katika Barabara Kuu inayoingia kutoka
mikoa kati, Hospitali ya Rufaa Bugando na kwenye ofisi za Chadema Kanda
ya Ziwa zilizopo kona ya Bwiru.
Mawazo aliuawa Novemba 14 baada ya kuvamiwa na kundi la
watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM na tayari watu watano wamefikishwa
mahakamani kwa kosa la mauaji.
Comments
Post a Comment