Rais Magufuli awasimamisha kazi Mkurugenzi, M/kiti wa Bodi ya Bandari (TPA) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi


Rais John P. Magufuli leo amevunja Bodi ya Bandari ya Jijini Dar es Salaam, kutokana na kashfa ya upotevu wa makontena ulioisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya Shilingi.
Mbali na kuvunja bodi hiyo, pia ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Prof. Joseph Msambichaka na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwinjaka.
Maamuzi hayo yametolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kwa niaba ya Rais ambapo amenukuliwa  akisema maamuzi hayo ya Rais yamekuja muda mfupi baada ya kubaini kasoro nyingi za kiutendaji kwa watumishi hao wa Serikali.
Pamoja na mambo mengine, amesema Rais amewasimamisha kazi maofisa nane kutoka Bandari ya Dar es Salaam baada ya kubainika walihusika kwa namna moja ama nyingine katika sakata hilo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mara baada ya agizo hilo, ameagiza wahusika wote wakamatwe na wawekwe chini ya ulinzi ili kusaidia upelelezi ikiwa ni pamoja na kueleza makontena yaliyopotea yalikuwa ya nani na yalikuwa na thamani ya shilingi ngapi.
Watuhumiwa hao watatakiwa kuwezesha makontena hayo yaweze kulipiwa kodi kutokana na awali kutolipiwa kodi.
Kwa upande wa suala la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebainika kwamba kulikuwa na matumizi mabaya ya fedha kiasi cha Sh. Bilioni 13 nje ya utaratibu ambapo uchunguzi zaidi juu ya fedha hizo unaendelea.
Hata hivyo, wakati wa tamko hilo, wahusika wote walikuwa hawapo wakati tamko hilo linatolewa na Waziri Mkuu.