Lugha za kuudhi, kuyumba kwa kiti cha Spika vyatia doa Bunge


Naibu Spika Dk Tulia Ackson. In Summary Mambo hayo kwa nyakati tofauti, yalisababisha wabunge kutolewa katika ukumbi wa Bunge kwa nguvu na hoja za msingi kutopewa muda wa kutosha wa kujadiliwa huku mawaziri wakibanwa kutokana na bajeti za wizara zao kuibua maswali mengi kuliko majibu. Dar/Dodoma. Kukithiri kwa lugha za kuudhi, vijembe, kuyumba kwa kiti cha Spika na bajeti kupita kwa mbinde, ni miongoni mwa mambo yaliyotikisa katika siku 19 tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti mjini Dodoma. Mambo hayo kwa nyakati tofauti, yalisababisha wabunge kutolewa katika ukumbi wa Bunge kwa nguvu na hoja za msingi kutopewa muda wa kutosha wa kujadiliwa huku mawaziri wakibanwa kutokana na bajeti za wizara zao kuibua maswali mengi kuliko majibu. Tathmini iliyofanywa na gazeti hili tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja vilivyoanza Aprili 19, imebaini kuwa mitafaruku mingi imeibuka katika siku ambazo kiti hicho kilikuwa kikiongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na Mwenyekiti, Andrew Chenge. Matusi bungeni Alhamisi iliyopita Mbunge wa Ulanga Mashariki (CCM), Goodluck Mlinga alizua sokomoko aliposema wabunge wa viti maalumu Chadema ni lazima waitwe ‘Baby’ ndipo wawe wabunge. Tafsiri ya kauli hiyo ni kuwa wabunge wa viti maalumu wa Chadema lazima wafanye mapenzi au kuwa na uhusiano wa kimapenzi na viongozi wa juu wenye mamlaka ndani ya chama hicho ndipo wateuliwe kuwa wabunge. Mbali na kauli hiyo, mbunge huyo huku akishangiliwa na wabunge wengi wa CCM, alisema ndani ya Chadema kuna wabunge wanaofanya mapenzi ya jinsi moja, kauli ambazo kwa kanuni za Bunge, zinaangukia kwenye lugha ya kuudhi. Licha ya wabunge wa upinzani kuchachamaa wakiomba mwongozo, kiti hakikumtaka mbunge huyo kufuta maneno hayo na badala yake Dk Ackson alisema pande zote mbili zimetumia maneno ya kuudhi hivyo yote yatafutwa kwenye kumbukumbu za Bunge hilo. Lugha hizo za kuudhi zilisababisha Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge alipotaka kumtwanga makonde Mbunge wa Kasulu Vijijini Augustine Holle (CCM) anayedaiwa kutumia lugha ya kuudh akisema Mnadhimu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ana cheti cha matibabu kutoka hospitali ya vichaa ya Mirembe, kauli ambayo baadaye aliifuta. Katika mwendelezo huohuo wa kauli za kuudhi kutokemewa, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka aliitwa mwizi ndani ya chombo hicho na baadhi ya wabunge wa upinzani bila kuchukuliwa hatua yoyote. Wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alisema wabunge wa upinzani wanataka kuonekana katika televisheni ili wapate wachumba. Akizungumza uendeshaji wa chombo hicho, Lissu alisema yanayotokea bungeni yanatokana na udhaifu wa kiti cha Spika akisema matamshi yaliyotolewa na Holle hayakuwa ya kibunge na kusema yaliendelea kwa sababu ya udhaifu wa kiti katika kusimamia kanuni za kudumu za Bunge. Uhalali wa mawaziri Kauli ya Lissu kuwa mawaziri wa Rais John Magufuli walitekeleza majukumu yao bila uhalali wowote wa kisheria ikiwamo kutumbua majipu Hata hivyo, Wazara wa Katiba na Sheria, Harrison Dk Mwakyembe alisema Rais anapoteua mawaziri kupitia ibara ya 55 ya Katiba, sharti muhimu ili waziri aanze kutekeleza majukumu yake ni kuapa mbele ya Rais na kwamba anaweza akakaa hata miaka mitatu bila kuwa na mwongozo na Serikali ikaenda. Mwanasheria Mkuu, George Masaju alisema sheria hiyo imetumia neno “the president may” akisema tafsiri yake ni kuwa anaweza lakini halazimishwi. Dk Ackson amuita mbunge bwege Oktoba 28 kulizuka mvutano mkali baada ya Dk Ackson kumtaka Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Saidi Bungara maarufu aache kuonyesha ubwege wake. Maoni ya wabunge Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alisema kiti cha Spika kinayumba kwa vile Naibu Spika hataki kusimamia kanuni ambazo ndizo zinapaswa kumuongoza. Mbunge wa Busega, Dk Raphael Chegeni(CCM), alisema kanuni ya 72 ya Kanuni za kudumu za Bunge inampa mamlaka Spika ya kufanya maamuzi kwa kadri anavyoona inafaa. Hata hivyo, alisema kanuni za 64,68 na103 zinawapa wabunge uwezo wa kuhoji au kutaka Spika azingatie matakwa yao. “Sasa kwa kuwa kanuni vilevile inataka busara na hekima ya Spika katika uendeshaji wa Bunge, basi kiti hicho kinaweza kuwa imara au kuyumba. Hali hii inaweza kabisa kutokea.” Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema Naibu Spika asipobadili aina ya uendeshaji Bunge na kwa kudhibiti kauli za kuudhi, chombo hicho kinaweza kupoteza heshima mbele ya umma.”