WATU 19 HUBAKWA NA KULAWITIWA KILA SIKU

Matukio ya ubakaji na ulawiti yanatajwa kushamiri kwa kasi ya ajabu, takwimu zinaonyesha kila siku watu 19 hubakwa na kulawitiwa.

Hali hiyo ni sawa na watu 570 wanaobakwa au kulawitiwa kwa mwezi au watu 6,840 kwa mwaka.

Hayo yalibainishwa Bungeni jana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe. Alisema hadi Machi, mwaka huu, mashauri yaliyopo mahakamani ni 2,031.

Hata hivyo, huenda matukio ya vitendo hivyo yakazidi kutokana na ukweli kuwa siyo kila anayefanyiwa ukatili huo huchukua hatua ya kufungua mashtaka katika vyombo vya dola.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (Tamwa) inadai ucheleweshaji na upotoshwaji wa ushahidi wa kesi za vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ubakaji na ulawiti katika ngazi ya mahakama, polisi na baadhi ya madaktari hospitalini.

Tamwa ilibainisha kuwa jumla ya kesi 62 za ubakaji zimeshindwa kutolewa hukumu au uamuzi na mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam katika kipindi cha 2014 hadi 2015.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa ni kesi moja tu ambayo mtuhumiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi 43 bado ziko mahakamani huku kesi 17 hazijafishwa mahakamani.

Mwanasiasa, Anna Abdallah alisema kushamiri kwa matukio hayo kunachangiwa na mmomonyoko wa maadili kunakoongezeka kwa kasi nchini.

Alisema katika baadhi ya maeneo, matukio ya ubakaji na ulawiti yanayofanywa na ndugu kwa kusukumwa na imani za kishirikina.