Ekari 56 za bangi zafyekwa

KAMATI ya Ulinzi na Usalama katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imeteketeza ekari 56 za
mashamba ya bangi.

Sambamba na hatua hiyo, pia kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga, imekamata magunia 20 ya dawa hizo za kulevya.
Kuteketezwa kwa mashamba na kukamatwa kwa bangi hiyo, kumetokana na msako mkali wa kupamba na na kilimo cha zao hilo wilayani humu uliofanyika kuanzia Februari 13, mwaka huu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu 14 wametiwa mbaroni na wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo.
"Nimeunda kikosi kazi kikishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani hapa cha kupambana, wakulima, wauzaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya ikiwamo mirungi kutoka nchi jirani ya Kenya," alisema.
Luoga alisema msako huo wa siku tatu, ulifanyika katika Kata za Mwema, Matongo na Kibasuka kwenye Vijiji vya Nyarwana, Matongo, Korotambe, Nyamohonda, Wegita na Nyakunguru.
Alisema bado wanaendelea kuwasaka watu wengine waliotoroka baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa 14 na kwamba kazi hiyo ni endelevu.
"Ninawaagiza viongozi wa vitongoji, vijiji, watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa kwa vyombo vya dola za watu wanaojihusisha na kilimo cha bangi, wauzaji wa dawa hizo za kulevya na wasafirishaji wake ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria kiongozi yeyote atakayeshindwa kutoa taarifa hizo katika maeneo yake atachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amewaonya wanaojihusisha na kilimo, usafirishaji na uuzaji wa dawa hizo za kulevya, waache mara moja na kuanzisha miradi mingine ikiwamo ya kilimo cha mazao ya chakula kama mahindi, migomba, viazi vitamu, vitunguu, alizeti na mboga.
Wilaya ya Tarime ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa katika kilimo cha bangi na soko kubwa la zao hilo liko nchi jirani ya Kenya na husafirishwa kwenda Mwanza na kuuzwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.