Eman Ahmed: Mwanamke mwenye kilo 500 apanda ndege, kupasuliwaMWANAMKE mmoja raia wa Misri, anayeaminika kuwa ndiye mwenye uzito mkubwa zaidi duniani, amewasili Mumbai , India ili kufanyiwa upasuaji.

Eman Ahmed Abd El Aty mwenye umri wa miaka 36 ana uzani wa kilo 500 ambaye anatakiwa
kufanyiwa upasuaji ili kumsaidia kupunguza uzito wake.
Safari hiyo, ilikuwa ya kwanza kwake kuondoka nyumbani katika kipindi cha miaka 25.
"Eman aliyesafiri kwa ndege ya EgyptAir aliwasili katika uwanja wa ndege wa Mumbai majira ya saa kumi alfajiri na akafika hospitalini Saifee mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri. Kitanda maalum alicholalia kiliinuliwa, akiwa kitandani kwa kutumia kreni," madaktari walisema.
Alisafirishwa kwenda hospitalini kutoka uwanja wa ndege kwa kutumia lori maalum lililofuatwa na gari la kuwabebea wagonjwa pamoja na gari la polisi.
Katika hospitali ya Saifee, kuna chumba kilichojengwa mahsusi kwa ajili yake.
Atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kufanyiwa upasuaji, madaktari wamesema.
Kwa sasa, atatunzwa na mtaalamu wa upasuaji Muffazal Lakdawala na kundi lake la matabibu, ambao wamekuwa wakimtunza kwa karibu miezi mitatu hata kufanikisha kusafirishwa kwake kutoka Misri.
Kutokana na ukweli kwamba hajatoka kitandani kwa miaka 25 iliyopita, alikuwa na hatari ya kuugua maradhi ya kupumua. Wakati akisafirishwa na madaktari walichukua tahadhari kubwa na kumpa dawa za kuyeyusha damu mwilini.
Kitanda alichosafirishwa nacho ni maalum kilichoundwa na mafundi wa Misri kwa kuzingatia matakwa ya shirika la ndege la EgyptAir.
Kilikuwa na mitambo na vifaa vya huduma ya dharura.
Familia ya Eman Ahmed inasema alikuwa na uzani wa kilo tano alipozaliwa kabla ya kupatikana na ugonjwa wa matende, ugonjwa ambao unasababisha kufura kwa mwili kutokana na maambukizi ya vimelea.
Wakati alipofikisha umri wa miaka 11, uzani wake uliongezeka maradufu na kuugua kiharusi ugonjwa uliomuacha kitandani kwa kipindi kirefu cha maisha yake.
Daktari wa upasuaji wa kupunguza matumbo kwa lengo la kutaka kupunguza uzani Muffazal Lakdawala hata hivyo aliambia BBC mwezi Desemba kwamba anaamini Eman Ahmed haugui ugonjwa wa matende bali anaugua ugonjwa wa kunenepa kupita kiasi ambao husababisha miguu kuvimba.
Ubalozi wa India mjini Cairo ulimkatalia kupewa visa bi Abd El Aty kwa kuwa hakuweza kusafiri pekee.
Alipewa visa baada ya Dk. Lakdawala kutuma ujumbe katika Twitter kwa waziri wa masuala ya kigeni nchini India Sushma Swaraj ambaye alijibu kwa kutaka kutoa usaidizi.
Upasuaji wa kupunguza matumbo ili kupunguza uzani wa mtu aliye na uzani mkubwa hutumika kama hatua ya mwisho ya kuwatibu watu walio na uzani mkubwa na walio na mafuta mengi.