Matumla Jr azirai kwa kipigo


Bondia Mohamed Matumla Jr amefanyiwa upasuaji wa kichwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kulazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU). Matumla Jr alipoteza fahamu akiwa ulingoni baada
ya kupigwa ngumi na bondia Mfaume Mfaume na kudondokea kichwa katika raundi ya saba ya pambano la raundi 10 la uzani wa light na kushindwa kwa TKO. Bondia huyo baada ya kudondoka ulingoni hakufanikiwa kuamka hadi alipofikishwa Hospitali ya Wilaya Temeke, alipatiwa huduma na kuzinduka kabla ya jana kuhamishiwa MNH. Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Chaurembo Palasa alisema Matumla Jr alihamishiwa Muhimbili ambako amefanyiwa upasuaji na kulazwa ICU. “Huenda akawa hospitali kwa siku tatu, itategemea na hali yake,” alisema Palasa licha ya baba mdogo wa Matumla, Mbwana kukiri bondia huyo kuumizwa katika pambano hilo lakini alisema hali yake si mbaya sana. “Mudy (Matumla Jr) hajambo kiasi ingawa alipoteza fahamu kwa muda baada ya pambano hilo na kupelekwa hospitali anakopatiwa matibabu,” alisema Mbwana. Kwenye pambano hilo lililofanyika juzi usiku uwanja wa ndani wa taifa, Dar es Salaam, hadi mabondia hao wanamaliza raundi tano za awali si mashabiki wa Matumla Jr wala Mfaume waliotarajia matokeo yatakuwaje kutokana na kushambuliana kwa zamu. By Imani Makongoro