Mnada Tanzanite waingiza mamilioni ya fedha


MNADA wa pili wa madini ghafi ya Tanzanite umeingiza dola za Marekani 4,202,287.13 baada ya kuuzwa
gramu 990,039.04


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bedera, alisema hayo katika hafla ya kuwatangaza washindi wa mnada wa madini hayo yaliyofanyika jijini hapa juzi.
“Inashangaza hivi sasa wachimbaji kuwapo urasimu katika kununua baruti kwa ajili ya uchimbaji wa madini, kwanini shirika moja tu la Mzinga ndilo liuze baruti hali inayosababisha ukata wa madini aina ya Tanzanite, ni kitu cha kushangaza katika zama hizi za utandawazi kuona biashara inamilikiwa na mmoja tu na kupelekea mateso kwa watumiaji wa bidhaa za baruti kwani wataalam wa migodi wanasema madini hayo hivi sasa yanapatikana kwa umbali mkubwa wa zaidi ya mita 1,000 kwenda chini," alisema.
Hata hivyo, alitoa rai kwa wachimbaji wa madini hayo kuwa na mpango mkakati wa kuendesha migodi kisasa ili kuwezesha kupatikana kwa urahisi madini na kupunguza ajali migodini.
Pia aliitaka Wizara ya Nishati na Madini kusimamia maslahi ya wafanyakazi migodini kwa kushirikiana na idara ya kazi.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema serikali itakaa na wadau wa madini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia ongezeko la kodi la asilimia 18 wanayotozwa Watanzania wanaposafirisha madini nje ya nchi, huku mgeni anayenunua madini hayo akitozwa asilimia 10 ya kodi.
“Kama kweli biashara hii inamnufaisha Mtanzania basi awekewe mazingira rafiki ya kulipa kodi na kuyauza nchi mbalimbali,” alisema.
Wizara ya Nishati na Madini imefanya mnada wa pili wa kimataifa wa madini ghafi ya Tanzanite na kampuni 68 zilijitokeza kununua madini hayo, huku 39 zikiwa ni za wazawa na 29 zikiwa zinatoka nchi mbalimbali duniani.
Katika mnada huo, kampuni tatu zinazochimba madini ya Tanzanite za Tanzanite one Mining Company Ltd, Mathias J. Lyatuu Mining na Tanzanite Africa Ltd zilipeleka jumla ya gramu 990,444.04 za madini ghafi na gramu 990, 039,04 za Tanzanite ghafi ziliuzwa na kuingiza dola za Marekani 4,202,287.13 sawa na asilimia 99.
Kupitia mnada huo, serikali imekusanya mrabaha wa dola za Marekani 210,114.36 sawa na zaidi ya Sh. bilioni 466, huku Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ikitarajia kulipwa Sh. milioni 27,987,232,.29 kama kodi ya huduma.