mwalimu aliyekacha kufundisha, anatengeneza viatuLicha ya kusomea taaluma ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Benjamin Ngowi hakukubali ajira aliyopewa na Serikali badala yake
akaitumia falsafa inayopigiwa chapuo na kujiajiri.
Amefanya hivyo kwenye eneo ambalo hakusomea bali kutokana na kipaji alichogundua kuwa nacho tangu akiwa mdogo. Ingawa hakitoshi, anayo mipango ya kukuza kipato chake ili kufanikisha ndoto alizonazo.
Benjamin ameamua kujiingiza kwenye ujasiriamali wa kutengeneza viatu na anabainisha kwamba huwa anauza kwa Sh25,000 kwa bei ya rejareja au Sh15,000 kwa bei ya jumla.
Anasema uwezo wake ni kutengeneza kati ya jozi 50 mpaka 70 za viatu kwa wiki ambazo hazikidhi soko lake. Ili kujiweka kwenye sehemu nzuri, amesajili kampuni yake ya Ngowi Production ambayo anatarajia itakuwa na matawi kwenye mikoa yote nchini.
Wakati Serikali ikitekeleza mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda, ipo hamasa ya kuwashawishi kuongeza ubunifu na kujiajiri ili kukabiliana na uhaba wa ajira uliopo nchini kutokana na kuongezeka kwa wahitimu kila mwaka.
Baada ya kuhitimu chuko kikuu mwaka juzi, Benjamin alipangiwa kazi katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro ambako hata hivyo hakwenda kuripoti licha ya kupata lawama nyingi kutoka kwa mama yake.
Anasema kutokana na mtazamo wa watu wengi kuamini zaidi kwenye kuajiriwa kuliko kujiajiri, mama yake pia hakukubaliana naye alipokataa kwenda kufanyakazi aliyosomea.
“Wakati vituo vya kazi vinatangazwa nilikuwa nimeshaanza kupata wateja wa kutosha hivyo ilikuwa vigumu kuacha shughuli niliyokuwa nayo hasa kutoka mikoa ya kusini,” anasema Ngowi..
Anasema alitumia muda mwingi kumshawishi mama yake aelewe anachokifanya kwani alikuwa anaamini katika kuajiriwa kwake kuliko kujiajiri jambo lililompa wasiwasi kwa kuhisi shughuli hiyo haitakuwa na faida na kuona mwanae anapoteza muda.
“Maneno ya watu ndiyo yalimpa wasiwasi kwani baadhi yao walidiriki kunipigia simu na kunishawishi nikafanye kazi niliyosomea,” anasema Ngowi.
Kutimiza malengo binafsi, uvumilivu na ustahamilivu unahitajika ili kukabiliana na changamoto zilizopo kabla ya kufikia mafanikio. Kutokana na haja ya kuboresha kipato, baadhi ya watumishi huacha kazi na kujiajiri ili kukidhi mahitaji wakati wengine wakiajiriwa na kujiajiri kwa wakati mmoja.
Benjamin, kijana mwenye umri wa miaka 27, mkazi wa Tabata Relini jijini Dar es Salaam anatumia kipaji chake cha kutengeneza viatu vya ngozi kabla hajamiliki kampuni ya ndoto yake na kuajiri vijana wenzake kuwahudumia Watanzania kwa bidhaa zenye ubora.
Ujasiariamali
Ari ya kujiajiri na kuajiri wengine ilimtia moyo na kumfanya aongeze juhudi ya kufanikisha adhima yake. Anasema utengenezaji wa viatu hajafundishwa na mtu yoyote bali ni kipaji kilichotokana na utundu wake akiwa mdogo.
“Nilikuwa na viatu nilivyovipenda ambavyo vilikuwa vigumu hata ngozi yake ilipoisha ngozi iliendelea kubaki na ilionekana bado mpya. Niliona naweza kufanya kitu, nilichukua begi langu lililokuwa limechakaa na kutengeneza viatu vya wazi kwa kutumia soli hiyo,” anasema Benjamin.
Baada ya kutengeneza kiatu cha kwanza, aliendelea kufanya hivyo na akafanikiwa kuuza jozi moja kwa mwanafunzi mwenzake jambo lililompa mwanga kuwa kuna fursa licha ya ugumu wa kupata soli kwa ajili ya kutengeneza viatu vingi zaidi hivyo akawa anatengeneza ‘key-holder’ ndogo na kuwauzia wanafunzi wenzake.
Akiwa kidato cha tano, aliendelea kutengeneza viatu na kuwauzia wanafunzi wenzake. “Kutokana na kukosa mtaji wa kununua ngozi, nilikuwa natengeneza kwa kutumia mabegi chakavu yaliyokuwa yakiuzwa kwa bei rahisi katika Soko la Karume,” anasema.
Kwa sasa anatengeneza kati ya jozi 50 mpaka 70 kwa wiki na wateja wake wakubwa wa jumla wanatoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Tabora.
Anasema mkakati wake ni kuimarisha ubora wa bidhaa zake ili kuwapa wateja wake kitu chenye thamani na kuongeza ushindani sokoni ambako kuna wazalishaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Ili kukabiliana na ushindani uliopo, anasema anapenda kujifunza kila aina mpya ya viatu inayoingia sokoni au mtandaoni kwa nia ya kukidhi ubora wanaotaka wateja wake.
Kama anayojifunza kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, anasema huitumia kutafuta wateja pia hasa kurasa zake za Facebook na Instagram.
Mpaka sasa ameajiri vijana wenzake wawili anaoshirikiana nao kwenye shughuli hiyo. Mmoja kati yao, Goodluck Lyamuya ambaye ni mhitimu wa stashahada ya masuala ya umeme anasema alihamasika baada ya kuona mwenzake amejiajiri na kuamua kuungana naye.
“Najivunia kufanya naye kazi kwani anapenda kuona vijana wenzake wakijishughulisha badala ya kukaa vijiweni bila kazi ya kufanya,” anasema Goodluck.
Mafanikio
Kutokana na shughuli yake, ameweza kubadilisha mazingira ya nyumbani kwao kwa kuweka umeme na kuboresha kilimo. Ana maduka mawili anayoyatumia kuuza na kusambaza bidhaa anazotengeneza.
Ili kuboresha bidhaa zake, amefanikiwa kununua cherehani ya kushonea viatu, mashine ya kupiga msasa soli na ya kulinganisha kuta za viatu. Haya yote ameyafanya kutokana na mtaji wa Sh300,000 alioanza nao.
Katika mipango yake ya muda mrefu, ana ndoto ya kufungua duka katika kila mkoa ili kuwafikia wateja wake na kuwavalisha Watanzania viatu vinavyotengenezwa ndani ya nchi badala ya vile vilivyotumika nje (mitumba).
Changamoto
Kutokana na kusomea masuala ya elimu, anasema alikuwa hana ujuzi wa ujasiriamali jambo lilimpa wakati wa kusajili wa biashara hivyo kulazimika kujifunza taratibu kadri siku zilivyozidi kwenda.
Upatikanaji wa malighafi ulikuwa ni jambo gumu kwani awali alikuwa anashindwa kutambua aina tofauti za ngozi na kuchukua ngozi duni na viatu alivyotengeneza vilionekana kukosa ubora.
Kutokana na kutokuwa na mafunzo na vifaa maalumu amekuwa akipoteza malighafi pindi alipokuwa anahitaji kutengeneza aina mpya ya viatu aliyoiona hivyo jozi ya kwanza ilikuwa ya majaribio kabla hajakamilisha aliyokuwa akiitaka.
Zana za uzalishaji zinauzwa ghali na kuwashinda wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa bora zitakazoshindana na za nje,” anasema.
Licha ya wajasiriamali, mamlaka kadhaa za Serikali zinaiona fursa iliyopo kwenye sekta ya ngozi hivyo kujitokeza na kuiendeleza. Mapema mwaka huu, Mamalaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade) kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) iliendesha semina ya kuwajengea uwezo wafugaji na wachinjaji wa kusindika ngozi za mifugo yao.
Semina hiyo pia ilikusudia kuwapa ujuzi wa kuziona na kuzitumia fursa zilizopo kwenye ngozi na bidhaa zake kwa kuwaelimisha wafugaji, wasafirishaji, wachinjaji na wasindikaji ili kuongeza thamani ya mazao hayo nchini