Waziri wa Afya 'apigwa mawe


KAMATI ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, imeikataa taarifa ya
Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, kuhusu hali ya dawa katika vituo mbalimbali vya afya nchini.Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo bungeni mjini hapa jana, Mwenyekiti wake, Peter Serukamba, alisema takwimu za taarifa hiyo kuhusu hali ya dawa katika vituo vya afya nchini, inatofautiana na takwimu zilizowasilishwa na wajumbe wa kamati yake. Aidha, Serukamba alisema kamati ilibaini kuwapo kwa deni la Sh. bilioni 154.8 inayodaiwa serikali ambayo imejipanga kulipa. Alisema kamati imebaini kuwa changamoto hiyo ya madeni yanaifanya MSD ishindwe kuagiza dawa za kutosha kwa wakati. Kadhalika, Serukamba alisema kamati imebaini Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umekuwa na utaratibu wa kuchagua baadhi ya magonjwa kugharimia matibabu yake. Alisema utaratibu huo wa kuchagua magonjwa ya kulipia huwakatisha tamaa wanachama kuendelea kuuchangia mfuko huo. BENJAMIN MKAPA Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeitaka serikali kufanya ukaguzi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyoko mkoani hapa inayokabiliwa na tuhuma za ufisadi na kupoteza ufanisi. Hatua hiyo inatokana na taarifa ya kamati hiyo iliyowasilishwa bungeni na Mwenyekiti wake, Serukamba aliyesema kuna ufisadi kwenye ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali hiyo. “Waziri alikiri katika maelezo yake alipokuwa akihitimisha na kuahidi kufanyia kazi suala hilo ikiwamo uchunguzi kufanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuleta taarifa mbele ya kamati, ”alisema Serukamba. Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), alisema kamati imebaini kuwa ukiacha changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, lakini kuna ufisadi mkubwa unaochangia ishindwe kujiendesha vizuri. “Kamati inaitaka serikali kufanya ukaguzi kubaini wahusika wa ufisadi huo na kuwachukulia hatua, pamoja na hayo kamati inashauri hospitali hii iwezeshwe kwa kupatiwa vifaa vya kutosha ili isaidie kutoa huduma kwa watumishi wanaohamia Dodoma,” alisema Serukamba. Kuhusu Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kamati imeitaka serikali kuhakikisha inaipa kipaumbele cha pekee kwa kuitengea fedha za kutosha. “Fedha zitolewe kwa wakati ili taasisi isaidie kupunguza gharama ambazo serikali imekuwa ikiingia kwa kuwapeleka wagonjwa wa moyo nchini India,” alisema Serukamba