Wema Sepetu akutwa na dawa za kulevya


Bangi imewekwa katika kundi la dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria za nchi. Kamanda Sirro alitoa
taarifa hiyo jana jijini Dar es Salaam katika siku ambayo vita dhidi ya dawa za kulevya nchini ilizidi kupamba moto baada ya jana Rais John Magufuli kuweka msisitizo. Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema katika vita dhidi ya biashara hiyo hakuna atakayesalimika hata akiwa mtu maarufu, waziri, mwanasiasa, askari au mtoto wa kigogo. Aidha, aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawakamata wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na kuwafikisha mahakamani hata kama ni mke wake, Janeth. Rais Magufuli alikuwa akizungumza baada ya kumuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venancy Mabeyo na Mnadhimu Mkuu wa jeshi hilo, Meja Jenerali James Mwakibolwa. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro alisema vijana wake wamewatia nguvuni jumla ya watuhumiwa 112 ambapo 12 kati yao walikutwa wakiwa na vidhibiti vya kete za madawa ya kulevya. Miongoni mwa waliokutwa na vidhibiti, alisema Kamishna Sirro ni Wema ambaye upekuzi nyumbani kwake jijini uliibua misokoto ya bangi pamoja na rizla ambazo ni karatasi za kusokotea bangi. Alisema upelelezi dhidi ya watuhumiwa 100 bado unaendelea na kwamba kwa 12 waliokutwa na vidhibiti wamefikishwa mahakamani. Alisema wataomba mahakama kuwaweka chini ya uangalizi kwa muda wa miaka miwili lengo ikiwa ni kuwafanya waache kuwa watumiaji wa madawa ya kulevya. SIKU YA SABA Harakati za kuwakamata watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika jiji la Dar es Salaam zinaendelea ikiwani siku ya saba tangu ambapo wasanii na watu maarufu mbalimbali wamekuwa wakihojiwa Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi. “Hakuna mtu maarufu, mwanasiasa, waziri au kiongozi yeyote au mtoto wa fulani, askari ambaye anajihusisha na dawa za kulenya aachwe, hata awe mke wangu Janeth... kamata wote weka ndani,” alisema Rais Magufuli. Alisema biashara ya dawa za kulevya kwa sasa nchini imefikia katika hali mbaya na kwamba zinauzwa kama njugu nchini. Alitaka vyombo vyote vya ulinzi vinavyoendelea kupambana na dawa za kulevya viendelee na mapambano. Alisema biashara ya dawa za kulenya kwa sasa nchini inapoteza nguvu kazi za Watanzania wengi haswa vijana, na kwamba vyombo vyote vya ulinzi vinapaswa kushirikiana ili kuwakamata hao. Hata hivyo, tofauti na jitihada za sasa ambazo zinaonekana kujikita katika kukamata watuhumiwa wa utumiaji, Rais Magufuli aliwataka wahusika kuuwinda mtandao wote unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya. “Haiwezekani wauzaji wapo mtaani wanatanua tu, hawakamatwi," alisema Rais Magufuli. "Kwa mfano kuna muuzaji mkubwa yupo mkoani Lindi, alishikwa na dawa za kulevya, lakini sijasikia hata siku moja akitangulizwa Mahakamani. "Ninajua kuna viongozi wanamtetea.” Rais Magufuli alikuwa akimzungumzia mtu anayeaminika kuwa 'mzungu wa unga' aliyekuwa akitafutwa zaidi nchini. Ali Khatibu Haji (47), maarufu kwa jina la Shikuba, alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Machi, 2014 baada ya kuwindwa kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa mkoani Lindi. Anatuhumiwa kuwa kiongozi wa genge lenye makao yake Afrika Mashariki, lakini likiwa na uhusiano wa kibiashara mpaka China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na Uingereza. Rais Magufuli alimwagiza Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuhakikisha kesi zote zinazohusu dawa za kulevya zinasikilizwa haraka. Imeandikwa na Gwamaka Alipipi na Halfani Chusi