Mrisho Mpoto Akiri Siasa Kuharibu Sanaa

WAKATI kila kona gumzo likiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, msanii wa Muziki wa Kughani Bongo,
Mrisho Mpoto amefunguka kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa imewaathiri wasanii katika kazi zao.
 Akipiga stori na Mikito Nusunusu, Mpoto alisema katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kwa muda mrefu gumzo limekuwa ni mambo ya kisiasa na mambo yanayomuhusu mkuu huyo wa Mkoa wa Dar na Askofu Gwajima hali ambayo imesababisha hata kazi za wasanii kukosa sapoti na kujikuta wakirudi nyuma kila kukicha.

“Wasanii tunategemea sana sapoti ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii lakini kwa sasa hatupati kabisa nafasi kwani unakuta msanii ametengeneza wimbo na video kali kwa gharama kubwa lakini hakuna anayeisapoti kwa sababu watu wanabaki kujadili mambo mengine ya kisiasa na haya mengine yanayoendelea hapa Dar, jamani hali hii imetuathiri sana kwa kweli,” alisema Mpoto.
Siku za hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda alitaja orodha ya wanaotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya ambapo Mchungaji Gwajima naye alikuwa mmojawapo na alipofanyiwa uchunguzi na kutoka kituo cha polisi, ‘Sentro’ ndipo gumzo lilianza kwani askofu huyo kila kukicha anakuja na kitu kipya kanisani kwake kuhusu mkuu wa mkoa hali inayosababisha mitandao na vyombo vya habari kupambwa na habari zao.