Raia Norway wanaongoza kuwa na furaha duniani


TAIFA la Norway hivi sasa ndiyo kinara wa kuwa na raia wenye furaha zaidi duniani, taarifa ya kitafiti ya Umoja wa Mataifa inabainisha.

Ripoti inayohusu furaha ya
umma duniani, inabanisha namna watu wanavyokuwa na furaha na chimbuko lake lilivyo.
Nchi nyingine tano katika orodha iliyoko ni pamoja na Denmark, Iceland, Uswisi na Finland ambazo ziko katika nafasi nzuri, huku Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiongoza kwa huzuni.
Mataifa ya Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini kwa sasa yameshikilia nafasi za juu, huku nchi maarufu duniani kama vile Marekani na Uingereza zikishika nafasi za 14 na 19 kutoka kileleni.
Umoja wa Mataifa unaorodhesha nchi zingine zenye furaha kama vile Uholanzi, Canada, New Zealand, Australia na Sweden.
Pia mataifa yaliyoko Kusini mwa jangwa la Sahara yako chini katika maisha ya raia wake kukosa furaha zaidi.
Ripoti hiyo inataja nchi ambayo raia wake wanaongoza kwa huzuni duniani au kokosa furaha ni Jamhuri Afrika ya Kati.
Zingine vinara katika hali hiyo, ni pamoja na Yemen, Sudan Kusini na Liberia.
Ni aina ya ripoti inayotokana na maswali ya kitafiti kwa watu zaidi ya 1,000 kutoka nchi 150 tofauti waliohojiwa ndani ya mwaka.
Miongoni mwa vigezo vilivyotumika ni ukaguzi wa pato la taifa, huduma za jamii, umri wa kuishi na uwepo wa rushwa.
Pia, ripoti hiyo ya mwaka huu inayojadili furaha ilikuwa na mada inayoangalia sababu za kushuka furaha nchini Marekani katika siku za karibuni.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Maendeleo Endelevu, Jeffrey Sachs, anasema kuna shaka kwamba chini ya uongozi na sera za Rais mpya, Donald Trump, mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi.
Wakati Norway iking’ara kwa kuwa na asilimia 75.5 ya furaha, watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wako katika wastani wa asilimia
26.9 ya furaha.