Taifa Stars Piga Hao Botswana

KIKOSI cha Taifa Stars, kikiongozwa na nahodha Mbwana Samatta leo kinacheza mechi ya kimataifa ya
kirafiki dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kimeahidi ushindi.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji iliyofuzu kucheza robo fainali ya Europa League, amesema pamoja na wachezaji wenzake watapambana kuhakikisha wanaifunga Botswana leo.
“Mimi na wachezaji wenzangu wote kwa pamoja tunatakiwa kuwaonyesha Watanzania kwamba hii mechi ni muhimu kwetu, hivyo tutapambana kuleta ushindi na itakuwa vizuri kwani tupo nyumbani,” alisema Samatta.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga, yeye alisema: “Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, ukiangalia vikosi vyote vina chipukizi wengi, hivyo tunatarajia mechi itakuwa nzuri kwa pande zote.
“Hii ndiyo mechi yangu ya kwanza nikiwa kocha mkuu, nimejipanga kufanya vizuri kwa sababu si mgeni na timu hii kutokana na kwamba huko nyuma nilikuwa kocha msaidizi.”
Wakati huohuo, Kocha wa Botswana, Peter Buffler, alisema: “Japo siwajui wachezaji wa Tanzania (Taifa Stars), lakini tumekuja kupambana nao kusaka ushindi, licha ya kuwa mchezo wenyewe ni wa kirafiki, ni muhimu kushinda na tunaamini tutafanya vizuri.”
Katika mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni, viingilio vitakuwa; V.I.P A Sh 15,000, V.I.P B Sh 10,000 na viti vya bluu, kijani na rangi ya chungwa ni Sh 3,000 tu.
na:  Sweetbert Lukonge