Wanaharakati 43 Misri wahukumiwa vifungo vya maisha

Misri. Mahakama ya Jinai ya Misri imewahukumu wanaharakati 43 wa
Kikundi cha Ikhwanul Muslimin, kifungo cha maisha jela kwa madai ya kushiriki maandamano dhidi ya Serikali.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana na mahakama hiyo, imesema wanaharakati hao walishiriki maandamano yaliyopigwa marufuku dhidi ya Serikali, kuwashambulia maofisa usalama na kupora mali za umma wakati wa maandamano hayo mnamo Desemba mwaka 2011.
Mbali na kuwahukumu kifungo cha maisha jela, mahakama hiyo imewapiga faini washtakiwa hao ya Sh 2bilioni kwa madai ya kupora mali za umma.
Wanaharakati wengine tisa wa Ikhwani wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela huku 92 wakiachiwa huru.
Baada ya Jeshi la Misri kumuondoa madarakani Mohammed Morsi mwaka 2013, Serikali ya Cairo ilipiga marufuku shughuli zote za wanaharakati hao.
Kadhalika idadi kubwa ya viongozi na wanachama wa harakati hizo zilizopigwa marufuku wamefungwa jela na baadhi yao wamehukumiwa adhabu ya kifo.