Breaking News: Manji Aachiwa Huru, Afutiwa Mashtaka ya Uhujumu Uchumi


MAHAKAMA ya leo Alhamisi, Septemba 14, imemuachia huru mfanyabiashara Yusuf Manji (41) na wenzake katika kesi ya uhujumu uchumi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) kuwasilisha hati mahakamani hapo ikionyesha kuwa hana nia ya kuendelea na kesi dhidi yake.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amewaachia huru washtakiwa hao saa saba mchana mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuiomba mahakama kufuta kesi hiyo chini ya Kifungu Namba 91 (i), cha mwenendo wa makosa ya jinai kinachompa mamlaka DPP kufuta kesi endapo ameona hana haja ya kuendelea nayo na mhakama ikaridhia.
Akiwasilisha ombi hilo mahakamani hapo, Wakili Kishenyi amesema kuwa leo yaani siyo tarehe ya kesi hiyo, ila waliomba hati ya wito ya mshtakiwa (Remove order) na kuiarifu Mahakama kuwa DPP kwa niaba ya jamuhuri  hakusudii  kuendelea  kuwashtaki washtakiwa  hao katika kesi hiyo  na akaomba iondolewe chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20.
Baada ya kueleza hayo,  Wakili wa washtakiwa hao, Hajra Mungula aliusema sheria hiyo inaruhusu DPP kuwaachia huru washtakiwa  na pia inaruhusu kuwakamata.
Hakimu Shaidi  kutokana na ombi hilo, aliwaambia washtakiwa hao kuwa mashtaka yamefutwa, wako huru  hivyo waondoke.
Katika kesi hiyo, Manji na wenzake Deogratius Kisinda (28), Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43), walikuwa wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na Usalama wa Taifa kwa kukutwa na mihuri na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200.
Mara baada ya kuachiwa huru, Manji aliulizia kuhusu malalamiko yake aliyoyawasilisha  mahakamani hapo kuhusu udiwani wake na Hakimu Shaidi alimueleza kwa kuwa yuko huru atalishughulikia hilo.
Manji alishaeleza kuhusiana na kutokubaliana na hatua ya kumvua udiwani iliyofikiwa na halmashauri ya manispaa.
Baada ya kuelezwa hayo Manji na wenzake waliondoka kwa kutumia gari moja  mahakamani hapo kuelekea  nyumbani kwao. Kesi  hiyo kabla ya kufutwa ilikuwa katika hatua  ambayo upelelezi wake ulikuwa bado haujakamilika na  ilipangwa kutajwa mahakamani hapo Septemba 18,2017.
Kwa mara ya kwanza kesi hiyo, ilisomwa Julai 15, 2017, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo Manji alikuwa amelazwa kutokana na matatizo ya moyo.
Kesi hiyo ilisomwa siku hiyo na wakili wa serikali Tulumanywa Majigo ambaye  alidai kuwa Juni 30, 2017 katika eneo la Chang’ombe ‘A’wilaya ya Temeke Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na bunda 35 za vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania zenye thamani ya Sh 192.5milioni na kwamba mali hiyoilipatikana kinyume cha sheria.