Kiba Aweka Rekodi Ya Mamilioni

 
 
WAKATI ukiwa na takriban siku 21 tangu kuachiwa sokoni, Wimbo wa Seduce Me wa mkali Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ unadaiwa kuweka rekodi ya aina yake kwa kumuingizia mtonyo usiopungua shilingi milioni 200.
Kiba aliuachia wimbo huo Agosti 25, mwaka huu ambapo kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, wimbo huo umemfanya Kiba aingize fedha hizo kutokana na shoo, mauzo ya miito ya simu na malipo mbalimbali ya mitandao.
“Huu ndiyo ukweli, najua watu wanaweza kukataa, lakini nakuhakikishia, mimi nipo karibu na uongozi wa Kiba, jamaa ameingiza fedha nyingi sana ndani ya muda mfupi. Ni rekodi ambayo kwa uzoefu wangu, hakuna msanii aliyeweza kuifikia kwa muda mfupi hivi.
“Mfano tu mdogo, kwenye shoo aliyofanya Marekani, pia wimbo huo umewekwa kwenye mtandao wa Vevo. Yaani kifupi ni zaidi ya hiyo milioni 200,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kuhakikishiwa taarifa hizo, Amani lilimvutia waya meneja wa msanii huyo Aidan Seif ambaye alikiri Kiba kupata mafanikio makubwa kupitia wimbo huo.
“Seduce Me kwa kweli imekuwa zaidi ya gumzo. Imeingiza hata zaidi ya hizo fedha ulizosema, kifupi ni mambo mengi.
“Shoo zimekuja nyingi za bei mbaya. Mitandao iliyoiingiza Seduce Me wanatulipa fedha nyingi sana, kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mungu,” alisema Seif.
Meneja huyo kutoka Lebo ya Rockstar4000, aliwashukuru Watanzania kwa sapoti kubwa waliyoionesha kwa Kiba na kuwaomba waendelee kuunga mkono muziki mzuri unaozalishwa katika lebo yao.
“Tunawashukuru sana Watanzania, wameonesha imani kubwa sana kwetu. Tunaomba waendelee kutuunga mkono, sisi tunaahidi kuwapa muziki mzuri,” alisema Seif.
Mbali na Kiba, Rockstar4000 inawasimamia wasanii wengine wakali akiwemo Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ na Omar Nyembo ‘Ommy Dimpoz’.