Tundu Lissu Avamiwa, Apigwa Risasi, Akimbizwa Hospitali


MBUNGE wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amevamiwa na watu wasiojulikana kisha kumpiga risasi zinazodaiwa kuwa tano.
Tukio hilo linadaiwa kutokea leo akiwa nyumbani kwake Area D Mjini Dodoma ambapo watu hao walimvamia akiwa kwenye gari kisha kumpiga risasi za miguuni na tumboni. Imeelezwa kuwa alikuwa akitokea Bungeni na alienda Nyumbani kula chakula cha mchana.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, amekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambapo amefikishiwa kwenye chumba cha upasuaji (theatre) na hali yake ni mbaya sana.
“Ni kweli, Tundu Lissu amepigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, amekimbizwa katika Hospitali ya Mkoa, Dodoma. Na mimi nipo njiani naelekea huko hospitali kumuona,” alisema Mbowe.