JPM ABAINI MADUDU TENA BANDARINI, ATEUA KAMISHNA WA MADINI

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Shukrani Elisha Manya Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kuwa Kamishna wa Madini.

Rais ametangaza uteuzi huo leo Jumatatu Januari 8, 2018 alipokuwa akitoa hotuba fupi mara baada ya kumuapisha Mhe. Dotto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini.

“Nimesikia tatizo ni kamishna wa madini, sasa nimeamua kumteua kamishna mpya wa madini, jina lake linaanza na Prof. Shukrani Elisha, huyo atakuwa ndiye mtendaji na msimamizi mkuu wa madini.
“Mambo ya hovyo ni mengi mno, nilipotembelea bandarini niliunda katume kasirisiri hivi, kwa kulihusisha Jeshi la Wananchi, TISS na Polisi. Yanayogundulika huko ni ya ajabu, kuna hadi simenti za zamani sana, yapo makontena bandarini na pale Ubungo.
“Mimi sio mwanasiasa mzuri wa kubembelezabembeleza, nikitoka mimi mtapata wakubembeleza, ila mimi nataka kabla ya Ijumaa regulations (kanuni za sheria ya madini) ziwe zimesainiwa. Pro Kabudi nendeni mkazifanyie kazi, tafuta watu wa kukusaidia na mkamalize hayo,” alisema Magufuli.