KISA KUNGUNI KWENYE NDEGE, GHANA YAIONYA BRITISH AIRWAYS

WAZIRI wa Mambo ya Anga wa Ghana, Cecelia Dapaah ameionya Kampuni ya Ndege ya Uingereza (British Airways) kwamba huenda ikakabiliwa na vikwazo kufuatia ripoti ya kunguni katika baadhi ya ndege zake zinazoingia nchini humo.
Gazeti la Uingereza wiki hii liliripoti kwamba ndege moja ya kampuni hiyo iliokuwa ikielekea mjini Accra ilizuiwa katika uwanja wa Heathrow kwa saa kadhaa baada ya wadudu hao kuonekana wakitambaa katika viti vyake.
British Airways ambayo ina ukiritimba wa ndege kati ya Uingereza na Ghana imetoa taarifa ikisema kuwa kisa kama hicho sio cha kawaida ma kundi la wataalam limechukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo.
Wahudumu hao walizua taharuki walipokurupuka nje badala ya kuwaelekeza wasafiri kuingia ndani ya ndege hiyo.
Gazeti la The Sun lilichapisha habari kuwa wahudumu wa ndani ya ndege hiyo walipigwa na butwaa walipowaona kunguni wengi tu ndani ya ndege na kulazimu kuahirishwa kwa safari yao.