MJAMZITO ATAKA KUJIFUNGUA KOPO

MWANZA: Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mama mmoja mjamzito aliyefahamika kwa jina la Vera Paschal (29), mkazi wa Kishiri, jijini Mwanza ameibua utata baada ya kudaiwa amejifungua kopo. Taarifa za awali zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa, mama huyo alifika kwenye Kituo cha Afya cha Igoma (pichani), akaomba ajifungue kopo kitendo ambacho kiliwashtua wauguzi waliokuwa zamu siku hiyo.
“Wauguzi walishangaa kweli, sasa mtu anasemaje anataka kujifungua kopo? Tulishindwa kuelewa kwamba ana akili timamu au vipi lakini kwa jinsi alivyokuwa akizungumza tulibaini anazo akili timamu,” alieleza mdau mmoja mtandaoni aliyedai alishuhudia tukio hilo. Hata hivyo, vyanzo vingine vilidai kuwa, mama huyo alikuwa na ugomvi na mumewe hivyo alifanya vituko vya kujifanya ana mimba akaficha kopo hilo karibu na sehemu za siri ili kumuonesha mumewe kuwa anataka kutoa mimba hiyo.

“Watu bwana, kuna wanaosema eti alikuwa ana ugomvi na mumewe. Sasa sijui katika kufanyafanya vituko, akaweka kopo sehemu za siri na kujifanya kama anataka kujifungua,” kilidai
chanzo. Kutokana na utata huo, Risasi Jumamosi lilifanya jitihada za kuzungumza na mganga aliyekuwepo zamu katika Kituo cha Afya Igoma, Zaituni Mkurunge ambapo alikanusha taarifa zilizokuwa zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Mganga wa Kituo cha Afya Igoma, Zaituni Mkurunge.

“Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikieleza kuwa kuna mama amejifungua kopo katika kituo chetu si za kweli, bali Jumatano (iliyopita) mchana majira ya saa 9:00 alasiri alikuja mama mmoja mjamzito akiwa amepakiwa kwenye Bajaj akilalamika kuwa anataka kujifungua kopo. “Lakini tulipompokea na kumpeleka katika chumba cha wazazi tulimpima na tukagundua kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi sita na tulipomchunguza vizuri kweli tulikuta kopo la mafuta ya kujipaka lenye ukubwa wa gramu 100 limeingizwa kwenye uke wa mama huyo.

Kopo linalodaiwa ndo hli
“Ikabidi tutumie utaalamu wetu kulitoa lile kopo ambapo tulichukua kama saa moja hivi na tukafanikiwa kulitoa, tulimuuliza hili kopo nani amekuingizia, alitujibu kuwa aliota usiku anaingiziwa kopo kwenye uke wake,” alisema muuguzi huyo. Akizidi kusimulia tukio hilo, muuguzi huyo alisema hawajawahi kukutana na tukio la namna hiyo ambalo wengine walilihusisha na mambo ya kishirikina.

“Tukio hilo lilitushangaza, sisi kama wauguzi hatuamini vitu vya kishirikina lakini mimba yake ipo na ule mlango wa uzazi ulikuwa bado haujafunguka. “Baada ya kumtoa lile kopo, tuliwaita polisi ili kufanya uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo lakini wito wangu kwa wakina mama wajawazito wasiwe na tabia ya kudanganya, wawe wanasema ukweli,” alisema muuguzi huyo. Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, Ahmed Msangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Tukio hilo lipo mikononi mwetu na uchunguzi unaendelea na itakapobainika kuwa mama huyo ana kesi ya kujibu, hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema