MZEE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU AFARIKI DUNIA

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Kingunge Ngombale-Mwiru amefariki dunia leo.
Taarifa kutoka kwa Mtoto wake Kinje Ngombale amethibitishaa kuwa Baba yake Mpendwa amefariki usiku wa kumakia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Kingunge Ngombale Mwiru ni Mkongwe wa Tanzania na jina lake ni kubwa. Ni mstaafu ambaye katika maisha yake toka ujana wake amelitumikia Taifa mpaka hata ngazi za juu kabisa kama vile kuwa Mkuu wa Mkoa, Mbunge na hata Waziri.
Ni mmojawapo wa vijana wa TANU enzi zao hizo, walioshiriki harakati za kuutafuta uhuru mpaka ukapatikana. Yeye kingunge ndiye aliyekabidhiwa jukumu la kuzigawa kadi mia za kwanza kabisa za wana TANU baada ya TANU kuanzishwa ambapo, Bwana Sykes ndiye aliyezichapisha kwa pesa za kutoka mfukoni mwake.
Kingunge alifanya harakati akiwa karibu na Mwalimu Nyerere, na waliendelea kuwa karibu hata baada ya uhuru kwa majukumu ya kujenga Taifa changa. Kingunge alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa na nafasi nyeti katika TANU na CCM mpaka pale alipoamua kuondoka CCM wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 na kwenda upande wa upinzani.
Mungu ailaze roho ya Mzee wetu mpendwa mahali pema peponi Ameni.